Вход на сайт

Просмотр новости

Найдите то, что Вас интересует

Usalama wa kihisia msingi muhimu utekelezaji wa mtalaa

Дата публикации: 10-08-2026 16:46:52

Mafunzo ya walimu jijini Dar es Salaam yalinikutanisha na simulizi la Mercy, mtoto wa miaka sita anayesoma darasa la pili katika shule moja ya msingi ya bweni. Kwa mara ya kwanza, nilikutana na Mercy miezi sita iliyopita. Familia yake inaishi mkoani Dodoma, kwa hivyo ilikuwa muhimu kumpeleka bweni kwa usalama wake.

Основное содержимое страницы с новостью.

Mafunzo ya walimu jijini Dar es Salaam yalinikutanisha na simulizi la Mercy, mtoto wa miaka sita anayesoma darasa la pili katika shule moja ya msingi ya bweni. Kwa mara ya kwanza, nilikutana na Mercy miezi sita iliyopita. Familia yake inaishi mkoani Dodoma, kwa hivyo ilikuwa muhimu kumpeleka bweni kwa usalama wake.

Kinyume na matarajio ya wazazi wake, Mercy anaishi maisha magumu mno yanayomfanya awe mnyonge. Ingawa shule ina kila anachokihitaji, kwa maana ya vifaa ya kujifunzia na mazingira salama ya kuishi, Mercy anaishi maisha ya upweke kama alivyonieleza, “Nataka kurudi kwa baba na mama. Sitaki kubaki hapa shuleni.” Kwa mujibu wa wazazi wake, Mercy ni mtoto mwongeaji. Hata hivyo, tangu ajiunge na shule hiyo ya bweni mwaka jana Mercy hana mengi ya kusema. Mzunguko wa wenzake anaoshirikiana nao hauoneshi kama anaamini watu kirahisi.

Tathmini ya ujifunzaji ninayofanya na Mercy inaonesha uwezo wa chini wa kutambua, kukumbuka, kufikiri na hata kujieleza kile anachoelewa. Ninapompa maswali ya kufanya kupima ustahimivu wake, Mercy hamalizi. Dakika tano zinaonekana kuwa nyingi kwake kukamilisha kazi nilizompa. Mercy hatulii na hawezi kuweka akili yake kwenye shughuli rahisi ninayompa.

Ninapojaribu kuzungumza naye, Mercy haonekani kuwa na uzingativu wala utulivu. Ingawa hasemi wazi lakini Mercy yu na hofu. Naambiwa hata matokeo yake ni mabaya na hali hii tayari inawatisha walimu. Simulizi la walimu wake linabeba sura ya mtoto mvivu asiyejituma.

“Huyu mtoto amelelewa kimayai sana nyumbani,” ananiambia Imani Madeleka mwalimu wake wa darasa na kuwatuhumu wazazi wake, “Hakufundishwa kujituma kabisa. Mvuvi na legelege. Darasani analala muda mwingi. Tumepambana kumnyoosha awe kama wenzake naona kama ndio anazidi kuwa mzembe.”

Salome Safari, mlezi wa bweni, tofauti na mwalimu wa darasa, hashangazwi na hali hiyo kama anavyoeleza, “Hawa watoto wa hivi (kama Mercy) tunao wengi hapa shuleni. Mwanzoni wanakuwa hivi lakini baadae tunawakomaza.” Namwuuliza ana maana gani anaposema kuwakomaza? “Kuwafundisha kuishi bila kukumbuka kumbuka nyumbani. Hawa wakifika darasa la tano hawataki hata kuwaona wazazi wao.” Ingawa mlezi anafikiri kumkomaza ni kumsaidia, kimsingi anachomaanisha ni kumfundisha mtoto kujitenga na familia yake kihisia. Tafiti zinaonesha kujitenga huku kunaweza kuweka rehani uwezo wake wa kutengamana na familia yake.

Ujifunzaji unafanyikaje?

Simulizi la Mercy linaibua maswali muhimu. Kwa nini mtoto mwenye uwezo mzuri wa kiakili anaweza kushindwa kufanya vizuri masomoni? Huu ‘uvivu wa mtoto’ unaolalamikiwa unatokana na nini na kipi kinaweza kufanyika kuurekebisha?

Kama walimu wa Mercy wanavyoeleza, walimu wengi hatuonekani kuwa na uelewa mzuri wa ujumbe unaobebwa na hisia za mtoto. Hatuoni uhusiano wa mmoja kwa moja kati ya hisia na ujifunzaji.

Lakini pia, kuna tatizo la kuichukulia elimu kama ‘kumpakia’ mwanafunzi maarifa na taarifa ambazo wakati mwingine hatumuandaa kuzipokea. Tunafikiri kujifunza kunahitaji maarifa kuingia kwenye akili ya mtoto. Hii ndio sababu mojawapo ya utamaduni wa bakora kama mbinu ya kuwalazimisha wanafunzi kukariri majibu.

Sayansi inasemaje? Kwanza kabisa, mtoto hawezi kujifunza kwa ufanisi ikiwa hajisikii kuwa salama. Usalama maana yake ni imani anayokuwa nayo mtoto kuwa yupo mtu mzima karibu naye anayepatikana kihisia, anayejali usalama wake, anayeheshimu anayekuchukua hatua pale anapogundua mtoto anakabiliwa na wasiwasi, hofu na chochote kinachotishia amani na utulivu wake. Usalama huu ndio unaoweka mazingira mazuri ya mtoto kujifunza.

Ubongo wa binadamu una sehemu mbili muhimu zinazowezesha ujifunzaji. Sehemu ya kwanza,  limbic system, huhusika na hisia. Kisayansi sehemu hii hukamilika mara tu shina la ubongo linaloshughulika na uhai ilipokamilika wakati mimba inapotungwa. Kazi yake kubwa ni kutambua tishio la usalama kwa kupiga ‘kengele ya hatari’ na kutoa amri ya kujilinda kwa kushambulia au kukimbia.

Sehemu ya pili, prefrontal cortex, huchelewa kukamilika hata baada ya mtoto kuzaliwa. Hiki ni kituo cha ubongo kinachofanya kazi kubwa ya kupokea taarifa, kuzichambua, kuzikumbuka, kujenga uelewa mapya, kufikiri, kudadisi na hata kutafuta ufumbuzi.

Sehemu hizi mbili hufanya kazi pamoja kwa utaratibu wa hisia zinaanza kisha kufikiri kunafuata. Tafsiri yake ni kwamba ili mtoto aweze kufikiri na kujifunza vizuri, lazima kwanza limbic system imhakikishie usalama wake. Katika mazingira ambayo mtoto hajisikii salama, ana wasiwasi, hana imani na watu waliomzunguka, sehemu inayohusika na kufikiri hupunguza uwezo wake wa kufanya kazi na hata kuzimwa kwa muda.

Matokeo yake ni kuzorota kwa uwezo wa mtoto kufikiri, kukumbuka na kudadisi. Ingawa kijuu juu mtoto anaweza kuonekana mvivu, asiyejali masomo wala kuelewa, lakini ukweli ni kwamba ubongo wake unakuwa umeingia katika hali ya kujilinda. Katika mazingira kama haya kujifunza kunakuwa si jambo muhimu.

Ushahidi wa kisaikolojia

Abraham H Maslow, mwanasaikolojia wa zamani alionesha kuwa nyuma ya tabia na maamuzi ya mwanadamu upo msukumo wa mahitaji fulani. Kinachoamua kile anachofanya mtu ni hitajji alilonalo wakati huo. Usalama, kwa mfano, ni hitaji la msingi kabla mtu hajawaza kujifunza, kufikiri na kujitambua. Mtoto anayejisikia yupo katika mazingira ya hatari, kama ilivyo kwa Mercy, hawezi kuelekeza nguvu zake kujifunza.

Tunapotazama ukweli huu katika mukhtadha wa elimu, tunaweza kuona mtoto anayeishi kwa hofu, fadhaa, aibu, msongo, au upweke hutumia nguvu nyingi kujilinda, kujihami na kujifariji badala ya kujifunza. Kuhofia kufanya makosa kunamuondolea utulivu, kunapunguza umakini wake, kumbukumbu yake inakuwa dhaifu na hata hama ya kujifunza inaondoka.

Kadhalika, tabia za mwalimu, katika mazingira haya, zinaweza kuzidisha tatizo hasa anapoonekana kuamini kuwa adhabu na vitisho vinasaidia. Unapomtisha mtoto ambaye tayari anapambana na upweke wake, matokeo yake ni kuzidisha kengele ya amygdala na hivyo kuifunga zaidi sehemu ya ubongo inayohusika na ujifunzaji.

Kwa upande mwingine, mtaala ulioboreshwa unasisitiza ujifunzaji darasani unaokuza mahiri za udadisi, ubunifu, fikra tunduizi, utatuzi wa matatizo na ugunduzi. Kudadisi, kwa mfano, kunahitaji mtoto ajisikie huru kujaribu, kuwa tayari kufanya makosa, na kujiuliza ‘kwa nini?’ na ‘kivipi? Ubongo unapokuwa na mahangaiko ya kupambana na tishio la usalama inakuwa vigumu mtoto kutumia uwezo wake kikamilifu. Matokeo yake mtoto anageuka kuwa ‘kondoo’ anayefuata maelekezo ya mwalimu badala ya kudadisi, kutafuta maarifa na kujenga uelewa mpana.

Mapendekezo

Elimu yenye maana kwa mtoto huanza na hakikisho la usalama. Mazingira yasipomhakikishia mtoto usalama wake, uwezo wake wa kufikiri na kudadisi huzorota na chochote tunachojaribu kukiingiza kwenye ufahamu wake hakiwezi kupokelewa kama tulivyoeleza. Je, mafunzo ya ualimu katika vyuo vyetu yetu yanawajengea uwezo walimu wa kuuelewa ujumbe unaobebwa na hisia wanazokuwa nazo watoto wetu? Tumewasaidia walimu kuelewa msukumo nyuma ya tabia za watoto na mbinu chanya za kutumia katika kumrekebisha mtoto? Matukio ya walimu kutumia mbinu zinazokuza hofu na uhasama na watoto bado yanasikika.

Kwa msingi huo, tuna mapendekezo mawili makubwa. Kwanza, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia iingize suala la “usalama wa kihisia wa mwanafunzi” kama sehemu rasmi ya viashiria vya ubora wa shule. Ingawa tayari tunao mpango wa ‘Shule Salama’ unaoendelea kutekelezwa kote nchini, ni muhimu mpango huu ujumuishe uelewa wa elimu ya hisia kama sehemu ya utekelezaji wake badala ya kukomea kwenye mifumo.

Kadhalika, ipo haja ya kuimarisha mafunzo endelevu kwa walimu waliopo kazini kuhusu jinsi ya kujenga usalama wa kihisia darasani, kutambua dalili za mtoto kutokujisikia salama na kutumia mbinu zinazopunguza hofu.

Mwandishi ni mhadhiri, mtafiti na mshauri elekezi wa sayansi ya ujifunzaji katika Chuo Kikuu cha Dodoma.

Схожие новости

#Наименование новостиТональностьИнформативностьДата публикации
1Mafundisho ya dini yanavyosahaulika katika malezi ya watoto05.6209-08-2026
2Hii hapa fursa kusoma AI, sayansi ya data bure Japan05.7212-08-2026
3Tumtazame mwanamke kama injini ya maendeleo08.5709-08-2026
4В кемеровской школе, куда первоклассница пришла с ножом, выявили нарушения0009-02-2021
5Школу в Казани, где произошла стрельба, охраняла вахтерша0011-05-2021
6Mahitaji ya huduma za moyo Comoro yaipa fursa JKCI05.412-08-2026
7Кузнецова обратится в МВД для проверки безопасности школ Татарстана0012-05-2021
8МИД РФ рассматривает работу НКО Италии, помогающей детям в Донбассе, как жест дружбы0010-06-2021
9Muhimbili yatenganisha pacha walioungana07.2310-08-2026
10В школе Нижнего Новгорода оперативно оказали помощь пострадавшим0011-03-2025

Классификация: . Схожих патентов: 0. Схожих новостей: 10. Тональность: 0. Информативность: 5.56. Источник: www.mwananchi.co.tz.