Вход на сайт

Просмотр новости

Найдите то, что Вас интересует

Mafundisho ya dini yanavyosahaulika katika malezi ya watoto

Дата публикации: 09-08-2026 07:51:17

Katika miaka ya hivi karibuni, mjadala kuhusu malezi ya watoto umejikita zaidi kwenye elimu, lishe, afya na matumizi ya teknolojia.

Основное содержимое страницы с новостью.

Jumapili, Agosti 09, 2026

By  Lilian Timbuka

Mhariri

Mwananchi Communications Ltd

Muktasari:
  • Tukumbuke kuwa mtoto hazaliwi akiwa anajua mema na mabaya. Hujifunza kupitia kile anachokiona, anachosikia na anachoelekezwa na watu wanaomzunguka.

Dar es Salaam. Katika miaka ya hivi karibuni, mjadala kuhusu malezi ya watoto umejikita zaidi kwenye elimu, lishe, afya na matumizi ya teknolojia.

Ingawa mambo hayo ni muhimu pia katika malezi ya mtoto,  kuna eneo ambalo wakati mwingine halipewi uzito unaostahili la  kumjenga mtoto kiimani.

Dhana ya kumjenga kiimani ni ili awe na dhamiri inayoweza kutofautisha lililo sahihi na lisilo sahihi hata pale ambapo hakuna anayemsimamia.

Tukumbuke kuwa mtoto hazaliwi akiwa anajua mema na mabaya. Hujifunza kupitia kile anachokiona, anachosikia na anachoelekezwa na watu wanaomzunguka.

Ndiyo maana wazazi na walezi wanabeba jukumu kubwa la kumjengea msingi imara wa maadili utakaomwelekeza katika kila hatua ya maisha yake.

Na miongoni mwa nguzo muhimu zinazoweza kumlea mtoto mwenye utu, nidhamu na uwajibikaji ni malezi ya kiimani na kiroho.

Malezi ya kiimani hayamaanishi tu kumpeleka mtoto ibadani au kumkaririsha mafundisho ya dini. Ni mchakato wa kila siku wa kumfundisha kuishi kwa misingi ya ukweli, uaminifu, heshima, huruma, uvumilivu na kuwajibika kwa matendo yake.

Hivyo, mzazi anapaswa amjengee mwanawe msingi wa maadili hayo tangu akiwa mdogo, ili awe na uwezo mkubwa wa kukabiliana na changamoto za maisha bila kuyumbishwa kirahisi na shinikizo la mazingira.

Leo hii watoto wanakua katika dunia iliyojaa taarifa nyingi kuliko wakati mwingine wowote katika historia. Kupitia simu janja, televisheni na mitandao ya kijamii, wanakutana na mawazo, tamaduni na mitazamo mbalimbali kila siku.

Baadhi ya maudhui hayo yanawajenga, lakini mengine yanaweza kuwashawishi kuamini kuwa mafanikio yanapatikana kwa njia za mkato, kwamba ukosefu wa heshima ni jambo la kawaida au kwamba umaarufu ni muhimu kuliko tabia njema.

Katika mazingira ya namna hiyo, mzazi hawezi kuwa mlinzi wa mtoto kwa saa 24 kila siku. Anachoweza kufanya ni kumjengea mtoto dira ya ndani itakayomsaidia kufanya uamuzi sahihi hata akiwa peke yake.

Wataalamu wa malezi wanasema dira hiyo ndiyo inayojengwa kupitia malezi ya kiimani na kiroho.

Hata hivyo, Sifuni Kajuna, mtaalam wa saikolojia ya watoto anasema mafundisho hayo hayatakuwa na matokeo ikiwa hayatatafsiriwa katika matendo.

Anasema watoto hujifunza zaidi kwa kuiga kuliko kwa kusikiliza maelekezo. “Mzazi anayesisitiza uaminifu lakini akafanya udanganyifu mbele ya mtoto, au anayehubiri upendo huku akitumia lugha ya matusi na dharau nyumbani, humchanganya mtoto kuhusu maana halisi ya maadili. Kwa mtoto, maisha ya mzazi ndiyo somo la kwanza kabisa,” anasema Kajuna.

Anasema malezi ya kiimani yanapaswa kuambatana na mazungumzo ya wazi ndani ya familia. Wazazi wasisubiri mpaka mtoto afanye kosa ndipo waanze kutoa nasaha.

Kutokana na kauli ya mtaalamu huyo, ni wazi kwamba mzazi unapaswa kutambua kuwa kuna umuhimu wa kutenga muda wa kuzungumza na mtoto kuhusu changamoto anazokutana nazo shuleni, mitandaoni na katika makundi ya marafiki zao.

Mazungumzo hayo yatasaidia kumjengea uaminifu na yanaweza kumfanya awe tayari kushirikisha familia yake anapokumbana na vishawishi au matatizo.

Taasisi za dini nazo zina nafasi muhimu katika safari hii. Kupitia mafundisho, vikundi vya watoto na vijana pamoja na shughuli za kijamii, watoto hupata fursa ya kujifunza umuhimu wa upendo, ushirikiano, msamaha na kuwajali wengine.

Hata hivyo, jukumu la taasisi hizo haliwezi kuchukua nafasi ya wazazi. Msingi wa maadili hujengwa nyumbani, huku dini ikisaidia kuuimarisha.

Pia ni muhimu watoto wafundishwe kwamba imani ya kweli haiishii katika ibada pekee, bali inaonekana katika namna wanavyowatendea watu wengine. Mtoto anayeheshimu walimu wake, anayesema ukweli, anayewasaidia wenzake na anayewajibika kwa makosa yake anaonyesha matunda ya malezi bora ya kiimani. Hayo ndiyo maadili ambayo jamii inayahitaji ili kujenga kizazi chenye uwajibikaji na mshikamano.

Katika jamii yenye dini na tamaduni mbalimbali kama Tanzania, malezi ya kiimani yanapaswa pia kuwafundisha watoto kuheshimu tofauti za wengine.

Tukumbuke kumlea mtoto mwenye imani hakumaanishi kumjengea misingi ya ubaguzi au chuki, bali ni kumfundisha kuthamini utu wa kila binadamu, kuishi kwa amani na kushirikiana na watu wenye mitazamo tofauti. Huo ndio msingi wa kujenga familia ana taifa lenye umoja na utulivu.

Hakuna mzazi anayetarajia mtoto wake aje kuwa mtu asiye na maadili. Lakini maadili hayaoti yenyewe. Yanapandwa kwa maneno, yanamwagiliwa kwa matendo na yanakomaa kupitia mwendelezo wa malezi.

Hivyo, pamoja na jitihada za kuwatafutia watoto elimu bora na maisha mazuri, tusisahau kuwajengea urithi usioharibika wa maadili unaotokana na imani na malezi ya kiroho.

Mwisho wa yote, mafanikio ya mtoto hayatapimwa kwa vyeti atakavyopata au mali atakazomiliki pekee, bali pia kwa namna atakavyowatendea wengine na uamuzi atakaoufanya katika maisha yake.

Mtoto mwenye elimu bila maadili anaweza kuwa hatari, lakini mwenye elimu inayoambatana na msingi imara wa kiimani na kiroho huwa baraka kwa familia, jamii na taifa. Ndiyo maana kila mzazi anapaswa kujiuliza; pamoja na kumwandalia mtoto maisha bora, je, ninamjengea pia moyo wa kuwa mtu mwema?

Схожие новости

#Наименование новостиТональностьИнформативностьДата публикации
1Mafanikio darasani yanaanzia kwenye afya ya mwili07.8310-08-2026
2Sababu Tanzania kutunga sera mpya ya sayansi, teknolojia na ubunifu07.310-08-2026
3Usalama wa kihisia msingi muhimu utekelezaji wa mtalaa05.5610-08-2026
4Минпросвещения заявило о росте доступности дошкольного образования с 2019 года на 20%0012-07-2021
5Как провести время в гаджетах без вреда для здоровья 📱 ...0502-07-2026
6Кузнецова считает необходимым создать условия для занятий детей вместо запретов концертов0010-12-2018
7Число обращений к детскому омбудсмену Москвы по поводу образования выросло вдвое0027-11-2020
8Mehmet Emin Ay Anlatıyor: Çocuklarımıza Allah Teala'yı Nasıl Anlatmalıyız?010.7412-08-2026
9Священник Матуш Спишак (Словакия): «Лицемерие отталкивает от Церкви»5328-06-2026
10MTС AdTech: 63% россиян тратят на репетиторов для детей до 60 тыс. рублей в год0014-08-2025

Классификация: . Схожих патентов: 0. Схожих новостей: 10. Тональность: 0. Информативность: 5.62. Источник: www.mwananchi.co.tz.