Вход на сайт

Просмотр новости

Найдите то, что Вас интересует

Migogoro inapogeuka rafiki wa ndoa

Дата публикации: 09-08-2026 08:05:37

Soma zaidi...

Основное содержимое страницы с новостью.

Prime

Jumapili, Agosti 09, 2026

Muktasari:
  • Wengi huamini kuwa ndoa yenye furaha ni ile isiyo na mabishano, tofauti au msuguano. 

Dar es Salaam. Kwa muda mrefu, migogoro imekuwa ikichukuliwa kama ishara ya kushindwa kwa ndoa au uhusiano. Katika jamii nyingi, wenza wanaogombana huonekana kama waliopoteza upendo, heshima au mwelekeo wa pamoja. Wengine huamini kuwa ndoa yenye furaha ni ile isiyo na mabishano, tofauti au msuguano. 

Lakini utafiti wa kisasa wa uhusiano unaibua ukweli tofauti kabisa: si migogoro inayoharibu ndoa, bali ni namna migogoro inavyoshughulikiwa. Kwa mujibu wa mtafiti mashuhuri wa ndoa, Dk John Gottman, migogoro ni sehemu ya kawaida na isiyoweza kuepukika katika uhusiano.

 Kupitia utafiti mwingi aliofanya kwa miongo kadhaa, aligundua kuwa karibu kila ndoa ina migogoro ile ile inayojirudia, mara nyingi ikitokana na tofauti za tabia, maadili au mitazamo ya maisha. Kinachotofautisha ndoa zinazodumu na zile zinazovunjika si ukosefu wa migogoro, bali ni uwezo wa wanandoa kuishi na tofauti hizo kwa heshima.

Anabainisha wazi katika maandiko yake: “Migogoro mingi katika ndoa haiwezi kutatuliwa, bali inaweza kusimamiwa.” Kauli hii inaondoa shinikizo la kutafuta suluhu kamilifu kwa kila tatizo, na badala yake inaleta mtazamo wa uhalisia. Migogoro inapochukuliwa kama sehemu ya safari ya pamoja, badala ya tishio, wanandoa huanza kujifunza kutoka kwake.

Kwa mtazamo wa kisayansi, migogoro hutoa fursa ya kufichua mahitaji ya ndani, hofu, na matarajio yasiyosemwa. Pale ambapo migogoro inakandamizwa au kuepukwa, uhusiano hukosa ukweli na uhalisia.

 Lakini inapokabiliwa kwa uwazi na usalama wa kihisia, migogoro huwa daraja la kuelewana zaidi, si ukuta wa kuwatenganisha wenza.

Simulizi ya ndoa ya Debora na migogoro

Simulizi ya mwalimu Debora Michael, inashtua na kushangaza. Hii ni simulizu ya miaka 12 ya ndoa yake ambayo ameiendesha kwa kanuni ya kipekee ya ugomvi na vipigo akiamini ndio ndio nguzo ya upendo wao.

Kwa majirani na marafiki, maisha ya Debora ni uwanja wa vita na amekuwa akipigana vikali na mumewe hadi kufikia hatua ya kulazwa hospitalini mara kadhaa kutokana na majeraha. 

Hata hivyo, tofauti na wanawake wengine wanaokimbia ndoa za namna hiyo, Debora anasema hajawahi na hafikirii kabisa kumuacha mumewe.

"Ndugu, jamaa, marafiki pamoja na majirani walishanishauri sana niachane na mume wangu, wakawa wananiambia ipo siku ataniua lakini kiukweli, naenda kukaa nyumbani kwetu wiki moja tu, nahisi kama nimepungua kilo kwa mawazo hivyo narudi nyumbani kwangu kwa sababu nampenda mume wangu," anasema Debora.

Kisa hiki kinachukua mwelekeo wa kushangaza zaidi pale mwalimu huyu anapoeleza mtazamo wake kuhusu amani.  Kwake, ukimya na utulivu ndani ya nyumba ni ishara mbaya.

"Nimefikia mahali ambapo nisipogombana na mume wangu, nahisi kapata mwanamke mwingine wa nje kugombana na kununiana kulinifanya nione ndoa yangu ipo imara." 

Anasema akiona siku zimepita bila msukosuko, yeye mwenyewe hutafuta sababu ya kuanzisha ugomvi. Lengo la kufanya hivyo ni ili wagombane, kisha mume wake amfuate na kuanza kumbembeleza. 

Anasema kitendo hicho cha kubembelezana baada ya dhoruba ya ugomvi, ndicho kinachompa amani na kuifanya ndoa yao idumu kwa zaidi ya muongo mmoja sasa.

Kwa mwalimu Debora, migogoro na mume wake kwake ni fursa ya kudumisha uhusiano wao. Inawezekana kikawa kisa cha ajabu lakini ukweli unabaki kuwa si kila mgogoro ni balaa. Ipo migogoro inakujenga zaidi kwenye uhusiano.

Migogoro na mahitaji ya kihisia

Dk Sue Johnson, mtaalamu wa tiba za kihisia anaeleza kuwa migogoro katika uhusiano mara nyingi si kuhusu fedha, majukumu au malezi ya watoto, bali ni kuhusu hofu ya kihisia iliyojificha chini ya mada hizo. 

Anasema ugomvi mara nyingi ni kilio cha kuomba ukaribu, uthibitisho au usalama wa kihisia.

Katika kitabu chake:  Hold Me Tight, Johnson anaandika: “Migogoro ya uhusiano ni maandamano ya kihisia yanayouliza swali moja: Je, uko hapa kwa ajili yangu?” 

Kauli yake inaonyesha kuwa nyuma ya maneno makali au hasira, mara nyingi kuna hofu ya kupoteza uhusiano au kutothaminiwa.

 Migogoro inapochunguzwa kwa mtazamo huu, inabadilika kutoka kuwa vita hadi kuwa mawasiliano.

Dk Johnson anaeleza kuwa wenza wengi huingia katika mizunguko hasi ya migogoro, ambapo kila mmoja hujilinda badala ya kufunguka. 

Lakini pale wanandoa wanapojifunza kusikiliza hisia zilizo chini ya maneno, migogoro huanza kuwa chombo cha kuimarisha ukaribu. Anaandika tena: “Uhusiano huimarika pale wenza wanapojifunza kugeuza migogoro kuwa mazungumzo ya kuunganisha.”

Kwa mtazamo huu, migogoro haipaswi kuepukwa, bali kuelekezwa upya. Migogoro inapoendeshwa katika mazingira salama ya kihisia, hujenga uaminifu kwa sababu kila mwenza hujifunza kuwa anaweza kuwa mkweli bila kuachwa au kudharauliwa.

 Hapo ndipo uhusiano huanza kuwa wa kweli zaidi, wenye kina na uimara wa muda mrefu.

Mtazamo huu unaungwa mkono na tafiti zinazoonyesha kuwa wenza wanaoepuka migogoro kabisa mara nyingi huwa na umbali wa kihisia. Ukimya wa muda mrefu, badala ya amani, huweza kuwa ishara ya kujitenga. Migogoro inayoshughulikiwa kwa heshima, kinyume chake, huonyesha kuwa uhusiano bado una uhai na ni njia bora ya uwekezaji wa kihisia.

Migogoro kama njia ya ukuaji na ukaribu wa kina

Harville Hendrix, mwandishi wa Getting the Love You Want, anaeleza kuwa migogoro ina nafasi muhimu sana katika ukuaji wa mtu binafsi na wa uhusiano. Kwa mujibu wa nadharia yake,  migogoro hutokea pale ambapo majeraha ya zamani ya kihisia yanapoamshwa ndani ya uhusiano wa sasa. Badala ya kuona hili kama mkosi,  anachukulia ni fursa ya uponyaji.

Anaandika kwa maneno yenye uzito: “Migogoro katika uhusiano si ishara ya kushindwa, bali ni mwaliko wa kupona.” Tafsiri hii inaonyesha kuwa kila mgogoro hubeba ujumbe kuhusu hitaji la ndani ambalo halijatimizwa. Migogoro inaposhughulikiwa kwa ufahamu, wenza hujifunza si tu kuhusu mwingine, bali pia kuhusu nafsi zao.

Esther Perel, mwandishi wa kitabu:  Mating in Captivity, anaongeza mtazamo wa kipekee kwa kuonyesha kuwa migogoro pia huchangia kudumisha mvuto na nguvu ya uhusiano. 

Anaeleza kuwa uhusiano usio na msuguano kabisa huweza kupoteza uhai na msisimko. Anaandika: “Ukaribu wa kweli hauhitaji kukubaliana kila wakati; unahitaji uwepo na ujasiri wa kusema ukweli.” 

Tafsiri hii inaonyesha kuwa tofauti na migogoro vinaweza kuleta nguvu mpya katika uhusiano badala ya kuudhoofisha.

Perel anaeleza kuwa wenza wanaothubutu kukabiliana na migogoro kwa uwazi, hujenga heshima na kuvutiwa zaidi. 

Migogoro inapokuwa mahali pa kujieleza kwa uhalisia, uhusiano hupata kina ambacho hakiwezi kupatikana katika ukimya au kuepuka matatizo. Kwa mtazamo huu, migogoro ni sehemu ya kudumisha uhai wa kihisia na kimapenzi.

Kwa pamoja, mawazo ya Dk Gottman, DK Johnson, Hendrix na Perel yanaonyesha picha moja muhimu: migogoro si adui wa ndoa au uhusiano. 

Adui halisi ni dharau, ukimya wa kihisia, na kukosa usalama wa kuzungumza ukweli. Migogoro inayoshughulikiwa kwa heshima, huruma na ufahamu huimarisha uhusiano kwa kuujenga juu ya misingi ya uhalisia.

Katika mtazamo wa kisasa wa kisayansi, migogoro si jambo la kuogopa, bali ni rasilimali ya uhusiano. Inatoa nafasi ya kukua, kuelewana, na kujenga uhusiano ulio imara zaidi kuliko ule unaojengwa juu ya kuepuka matatizo.

 Ndoa au uhusiano usio na migogoro si lazima uwe bora; mara nyingi huwa ni uhusiano usiozungumza ukweli.

Migogoro inapokubaliwa kama sehemu ya safari ya pamoja, wenza huacha kuuliza, “Kwa nini tunagombana?” na kuanza kuuliza, “Tunaweza kujifunza nini hapa?” 

Ndani ya swali hilo, ndipo nguvu ya uhusiano huanza kujengwa upya. Katika dunia inayotafuta uhusiano kamilifu usio na msuguano, sayansi inatukumbusha ukweli muhimu: migogoro, inaposhughulikiwa vyema, si dalili ya mwisho wa upendo, bali ni ishara ya uhusiano unaokua.

Makala haya yametokana na vyanzo mbalimbali vya kimtandao.

Схожие новости

#Наименование новостиТональностьИнформативностьДата публикации
1Ijue siri ya kisukari iliyojificha kwenye wali, ugali01007-08-2026
2Kukosana katika ndoa ni fursa kwa wenza, msinune01009-08-2026
3Hii hapa sababu kukosa usingizi ukiwa na uchovu08.107-08-2026
4Ongezeko la wahitimu wa vyuo, wadau watoa pendekezo01010-08-2026
5Hivi ndivyo mwanachuo anaweza kujiajiri01012-08-2026
6Ulaji, mazoezi silaha magonjwa yasiyoambukiza01007-08-2026
7Mashindano ya Feassa yafunga shule Morogoro Mjini, ikiibua sintofahamu01010-08-2026
8Así te quedas sin amigos-5314-07-2026
9Newsletter exclusive: I was shocked when I found TWELVE of my middle-aged female friends have had affairs... and their husbands are clueless. But it's when they told me their five shameless rules to get away with it that my jaw truly dropped...-2321-04-2026
10Ez bilatu arrazoirik0022-10-2018

Классификация: . Схожих патентов: 0. Схожих новостей: 10. Тональность: 0. Информативность: 10. Источник: www.mwananchi.co.tz.